Kwa nini naadhimisha Tanzania?

Alama maalumu kwa ajili ya sherehe za kutimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara)

KWA haraka haraka kabisa mtu anaweza kukimbilia na kusema “Tanganyika”. Na sababu iko wazi kwamba nchi iliyopewa uhuru Desemba 9, kutoka udhamini wa Umoja wa Mataifa uliokuwa chini ya Mwingereza, iliitwa Tanganyika. Na ni kweli taifa lililokuwepo baadaye hadi wakati wa Muungano wa Aprili 26, 1964 liliitwa Tanganyika. Ni kweli walikuwepo raia wa Tanganyika na nchi inayoitwa Tanganyika. Kwa hiyo, kiufundi na kimantiki ni sahihi kusema kuwa ni “uhuru wa Tanganyika”. Ukiishia hapo utafanya makosa.

Tanganyika ni nini hasa?

Tanganyika ni zao la mkoloni. Tanganyika haikuwa zao la kina Sina, Meli, Mirambo, Mkwawa, Nduna Songea, Abushiri au tawala nyingine zozote za jadi. Tanganyika halikuwa zao la watu wa asili ya Tanganyika. Hata jina lenyewe limekuja kutoka ngwe ya kwanza ya karne ya 20 kabla ya hapo jina Tanganyika halikuwapo kabisa. Watu wa Tanganyika waliitangulia nchi ya Tanganyika.

Kabla ya ujio wa Mwingereza eneo hili kwa kiasi kikubwa lilijulikana wakati wa Mjerumani kama Afrika ya Mashariki ya Mjerumani. Kwa watu ambao hawajui, mipaka yake ilijumuisha nchi za Burundi, Rwanda na eneo la sasa la Tanzania bara. Ni baada ya vita ya kwanza ya dunia Ujerumani ikaondolewa (kama matokeo ya vita) na eneo lililokuwa chini ya Mjerumani zikagawanywa kwa Uingereza (Tanzania bara), Burundi na Rwanda chini ya Ubelgiji. Kwa maneno mengine, Tanzania bara ikiungana na Rwanda na Burundi leo tutakuwa hatufanyi kitu kipya kwani tumewahi kuwa chini ya utawala mmoja.

Hivyo, Mwingereza ndiye aliyeanza kuitawala Tanganyika na kuihudumia Tanganyika na wananchi wa eneo hilo kuanza kuitwa “Watanganyika”. Ikumbukwe kuwa kuunganishwa kwa Watanganyika hakukufanywa na Mwingereza na Mjerumani bali kuliunganishwa na wananchi wa maeneo hayo kwanza. Vita ya Majimaji ndio juhudi kubwa za kwanza zilizowaleta makabila ya bara ya eneo letu kwa pamoja kumpinga Mjerumani na utawala wa kigeni.

Hawakupigania ‘Tanganyika’; waliipinga ‘Tanganyika ya mkoloni’

Mababu wakati wa vita ya Majimaji walipigana kuukataa utawala wa kigeni kati yao. Hadi vita inaisha watu karibu 300,000 walikuwa wamekufa (kwa vita, na njaa ya makusudi iliyosababishwa na Wajerumani). Kulazimishwa kujisalimisha kwa mashujaa wetu kulifanywa ili kuwalazimisha kuwa ndani ya utawala wa Tanganyika ya mkoloni na mababu wengine walikubali kufa kuliko kuwa huru chini ya mgeni (Isike, Mkwawa, Bushiri, mashujaa wa Maji Maji n.k).

Walichopigania ni utu wao na haki yao kuwa binadamu wenye tawala walizojiamulia wao siyo zilizoamuriwa na mgeni wasiyemjua mwenye tamaduni tofauti na zao. Wazee hawakutambua uhalali wa Tanganyika lakini walilazimishwa kuwamo ndani yake na kwa kweli, baada ya udhalimu wa Mjerumani wazee wetu waliogopa kabisa tena kuleta vurugu dhidi ya watawala wageni.

Nyerere na mashujaa wetu wa uhuru hawakuitaka Tanganyika ya mgeni

Hivyo, wazee wa mwanzo ambao walianza kuwa na vuguvugu la kisiasa walianza kutamani kuwa na nchi ya kwao wenyewe. Wengine walitaka maisha yawe bora zaidi katika utawala wa kikoloni na wengine wakaanza kufikiria nchi huru ya kwao. Wakati Nyerere anaingia kwenye jukwaa la siasa za Tanzania mbegu ya matamanio ya uhuru ilikuwa tayari imepandikizwa na uasi wa Wazanaki, vurugu za Mt. Meru na Mwanza na migomo ya makuli bandarini. Tayari kulikuwa na hamu ya njozi ya kuwa huru.

Wote – Nyerere na mashujaa wa zama zake walikuwa wanafanya kile kile kilichofanywa na baba zao miaka michache nyuma – kuikataa Tanganyika ya mkoloni. Walijua haitoshi kuwa na maisha mazuri, na kutambuliwa na wakoloni kuwa na wenyewe ni binadamu. Walijua haitoshi kuishi tu na wakoloni – walitaka kitu zaidi ya kile kilichoundwa na wakoloni.

Maana kama nchi ilikuwepo, mipaka ilikuwepo, jeshi lilikuwepo, Mahakama zilikuwepo na hata baraza la kutunga sheria. Lakini hivyo vyote havikuwafanya wajisikie wako kwenye ‘nchi yao’. Waliishi ndani ya Tanganyika lakini hawakujiona ni Watanganyika kwani walikuwa ni raia wa koloni la Uingereza.

Wazo la Tanganyika huru

Nyerere, Sykes, Rupia, Mhando, Tambaza na wengine wa zama zao waliona katika fikra zao Tanganyika tofauti na ile waliyoishi wao. Waliiona Tanganyika ambayo ina watu huru wenye utu na haki sawa. Waliona Tanganyika ambamo watoto wake wana nafasi sawa kama watoto wa kizungu na hakuna anayebaguliwa kati yao.

Waliona kuwa hakukuwa na sababu ya msingi ya kwa nini wageni waamue kuhusu maisha ya watu wengi wa nchi yao bila wao kushirikishwa, hivyo wakaanza kile kinachoitwa ‘harakati za kutaka kujitawala”.

Ghana na India zilipopata uhuru wazee wetu waliaminishwa kabisa kuwa wakati umefika na nchi hii kuwa huru vile vile. Kile ambacho naweza kukiita kuwa ni Tanganyika Mpya. Yaani, walitaka kuiondoa Tanganyika ya Mkoloni na kuunda Tanganyika ya Mtanganyika.
Hili hata hivyo ni lazima lieleweke. Wazee wetu hawakutaka Tanganyika ambayo iko huru lakini ikiwa inaendeshwa na mawazo na fikra za kikoloni. Walitaka Tanganyika kama nchi ambayo inaendeshwa na fikra na maslahi ya Watanganyika wenyewe bila kuamuliwa London na New York. Walitaka haki ya “kujiamulia mambo yao wao wenyewe”.

Walitaka zaidi ya Uhuru

Bahati mbaya sana watu wengi – hasa vijana wa leo ambao hawataki kurudi kujifunza historia – wanafikiria tulitaka ‘uhuru’ ili tuwe Tanganyika tu. Kwamba labda wazee wetu walitaka uhuru ili tujiite “Tanganyika’ na sisi tuseme ni Tanganyika. La hasha! Uhuru wetu ulikuwa unafungamana na uhuru wa Bara zima la Afrika. Hili ni jambo muhimu kidogo kulifikiria. Kina Nyerere hawakutaka kupigania uhuru halafu tuupate halafu tubweteke huku mataifa mengine ya Afrika yako chini ya ukoloni.

Uhuru wetu ulikuwa pia ni sehemu ya harakati za Uhuru katika bara la Afrika na tuliamini sisi kuwa huru kungesaidia kuweka msukumo kwa nchi nyingine (Zambia, Kenya, Uganda, Malawi na nyinginezo ambazo hazikuwa huru bado). Uhuru wa Tanganyika hivyo ulifungamana na Uhuru wa Afrika na wazee wetu walitambua hivyo. Ndio maana kulikuwa na kushirikiana kwa wanaharakati wa uhuru kutoka Kenya na Zimbabwe (Rhodesia) na hata kati ya wazee wa Tanganyika na wale wa Zanzibar. Wengine wanafikiria Tanganyika na Zanzibar zilianza kuhusiana kisiasa baada ya Muungano kumbe watu wa sehemu hizo wameshirikiana kisiasa hata kabla ya Nyerere kuingia katika siasa za Tanganyika.

Pamoja na uhuru wa Afrika, vile vile harakati za wazee wetu zilihusiana na Umoja wa Afrika. Wakati nchi za Afrika zinapigania uhuru vile vile zilikuwa zinapigania umoja wa Afrika. Wengi walitambua kuwa wakoloni ndiyo walimega mega jamii zetu na kutugawa na hivyo kurudia Umoja wa Afrika au jamii zetu tulikuwa tunarudia kitu chetu sisi wenyewe.

Wengi tunafahamu jinsi Wamasai walivyogawanyika kati ya Tanganyika na Kenya au Wajaluo kati ya Uganda, Tanganyika na Kenya au hata Wahaya kati ya Uganda na Tanganyika. Wakoloni kwa utawala wao waliivunja jamii yetu. Hivyo, harakati za uhuru zilihusiana vile vile na harakati za umoja.

Na ni kweli mwanzoni nchi kadhaa za Kiafrika zilijaribu kuurudisha umoja huu wa asili lakini pasipo mafanikio.
Hivyo, Tanganyika ilipopata uhuru Desemba 9, 1961, kwa watu wengine wanafikiria ilikuwa mwisho. Mzee yeyote au mwanahistoria yeyote anatambua kabisa kuwa tulipopata uhuru ndoto ya Tanganyika haikuwa imetimia. Bendi moja iliimba wimbo mashuhuru “Uhuru wetu hauwezi kuwa safi, mpaka Afrika yote imekuwa huru”! Tulitambua kama Watanganyika kuwa hatukupigania kuwa huru tu – tulipigania kuwa huru, na wamoja.

Siku chache kabla ya Uhuru Nyerere aliandika ujumbe huu kwenye gazeti la chama la Uhuru (lililotoka Sauti ya TANU) “Nina uhakika kuwa kila mmoja wetu atafurahia Siku ya Uhuru kwa furaha kubwa. Tunashangilia ushindi. Ni muhimu kukumbuka siku hiyo kuwa hata tulichojipatia ni haki ya kufanya mambo yetu sisi wenyewe, kubuni na kujenga maisha yetu wenyewe ya baadaye. Sawa na kujipatia ardhi ya kujijengea nyumba. Sasa kujipatia ardhi ya kujenga nyumba ni jambo la furaha lakini nyumba haitokei tu kwa kushangilia. Nyumba inahitaji nguvu zaidi, juhudi zaidi, jasho na uvumilivu kama ije kuwa sababu ya majivuno kwa walioijenga.” Hili ni kweli, siku ya Uhuru tulichofanya siyo kuipata Tanganyika tuliokuwa tunaitaka.

Akihutubia Baraza la Umoja wa Mataifa siku tano tu baada ya kupata uhuru Mwalimu Nyerere alielezea kuwa Tanganyika ilikuwa na kanuni nne ambazo ingefuata mojawapo ni kupinga ukoloni mahali popote na kwa namna yoyote ile. “Ni msingi wetu unaodumu wa kupinga ukoloni mahali popote kwenye bara letu na mahali popote duniani”. Tanganyika ilikuwa ni zaidi ya uhuru wa kujitawala ilikuwa ni wazo la nchi ya namna gani. Hotuba yake ya “A United States of Africa” ni mojawapo ya hotuba ambazo wachache wamezisoma lakini ni mojawapo ya hotuba ya falsafa ya hali ya juu ya Umoja wa Afrika.

Naomba niyaweke maneno ya mwisho ya hotuba hii ili watu waelewe ni kwa nini huwezi kuwaona wazee wa miaka ile ambayo wanaililia Tanganyika. Nyerere aliandika makala hii kwenye The Journal of Modern African Studies, Januari, 1963.
Anasema: A Federation of at least Kenya, Uganda, and Tanganyika should be comparatively easy to achieve. We already have a common market, and run many services through the Common Services Organization, which has its own Central Legislative Assembly and an executive composed of the Prime Ministers of the three states. This is the nucleus from which a Federation is the natural growth… One thing must be clear; once a Federation has been established by the will of the people it must not be allowed to break up again. It may expand or merge into a still larger unit, but its component parts will have made up a new body politic which cannot be chopped up. A Federation of East Africa must be well considered both for its own sake and because it must be a step towards total African Unity; once it has been established nothing must be allowed to fragment it.

Na Nyerere anamalizia makala hiyo kwa kusema maneno ambayo naomba msomaji ayafikirie:
Certainly, African Unity will not be easy to attain but equally certainly it can be won if the people of Africa so determine. As I have said once before, the role of African nationalism is different – or should be different – from the nationalism of the past. We must use Africa national states as an instrument for the reunification of Africa and not allow our enemies to use them as tools for dividing Africa. African nationalism is meaningless, is anachronistic, and is dangerous, if it is not at the same time Pan-Africanism.
Ukweli ni kwamba wazee wetu wakati wa kupigania uhuru na baada ya kupigania uhuru na kabla ya Muungano walitambua kuwa Tanganyika haikuwa nchi tu lilikuwa ni wazo ambalo liliunganisha haki ya kujitawala na umoja wa Afrika.

Tanzania kilele cha Tanganyika

Kwa mwananchi wa Tanganyika na hata sehemu nyingine za Afrika kutokea kwa Tanzania kulikuwa ni kwa asili. Kuliendana kabisa na njozi yetu ya nchi huru yetu wenyewe lakini vile vile kuliandana na hisia (sentiments) za harakati za uhuru kuwa uhuru wetu ulikuwa unaelekea umoja. Kimsingi kabisa Mtanganyika ni mtu wa kwanza Afrika kupigania Uhuru wa Afrika. Ni kweli Kwame na wazee wengine wa zama hizo walipigania “umoja wa Afrika” lakini ni katika Tanganyika umoja huo ulionekana na unaendelea kuonekana.

Kabla ya kujiunga na Zanzibar, Tanganyika ilikuwa tayari iko katika ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda na wengi mnafahamu jinsi ambavyo Nyerere alikuwa tayari hata kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili nchi zote za Afrika zipate uhuru pamoja na kuingia kwenye Shirikisho huku Mzee Kenyatta akiwa ni Rais wa kwanza. Wakosoaji wa Nyerere hawawezi kusema Nyerere alikuwa na kiu ya kutawala kwani ushahidi wa kihistoria uko wazi kwamba Urais kwake ilikuwa ni nafasi ya kutumikia tu siyo kitu cha lazima. Fikiria ni mwanasiasa gani leo ambaye anaweza kusema yuko tayari kuuachia “Urais” ili mtu bora zaidi atawale?

Tungeweza kabisa kuanza na nchi tofauti kabisa na ilivyo sasa yaani hata Tanganyika ya Tisa Disemba isingekuwepo. Fikiria kama Disemba 9, 1963 nchi za Kenya, Uganda, Zanzibar na Tanganyika zote zinapata uhuru na mara moja zinaunda Shirikisho la Afrika ya Mashariki. Hili nusura litokee. Na ingetokea wale wanaoililia Tanganyika wasingekuwepo kwa sababu watu wanacholilia ni Tanganyika iliyokuwepo kwa miaka kama mitatu tu toka Disemba 9, 1961 hadi Aprili 26, 1964.

Wazo la Tanzania lilibebwa katika Tanganyika ya 1961

Ndugu zangu, binafsi siadhimishi uhuru wa “Tanganyika” bali wa Tanzania. Siangalii tarehe au nchi iliyozaliwa tu naangalia wazo lililosababisha nchi hiyo kuwemo. Ninaamini Tanzania inakaribiana zaidi na wazo la harakati za uhuru kuliko Tanganyika tuliyojipatia 1961. Lakini zaidi ni kwamba Raia wengi zaidi leo hii ni Watanzania kuliko wale wailiokuwa Tanganyika. Wazee wengi waliishi katika Tanganyika ya mkoloni (1920-1961) ukilinganisha na wale waliozaliwa 1961-1964. Tena tunaweza kujenga hoja kuwa hakuna mtu mzima yeyote aliyezaliwa na kufa akiwa raia huru Mtanganyika (kwani Utanganyika ulidumu kwa miaka 3 tu!)

Hivyo basi tunapoadhimisha mika hamsini ya Uhuru tunaadhimisha miaka hamsini ya wazo la Tanzania. Ni sawasawa na kutungwa mimba kwani wazo la Tanzania lilitungwa mimba 1961 na kuzaliwa Tanzania na kama tunavyoelekea na kurudia misingi yetu tunaweza kujikuta tunauna lile Shirikisho la Afrika ya Mashariki ambalo ndio kilele cha harakati za uhuru. Tanganyika haikutakiwa iwe mwisho na hakuna wakati wowote wa uhuru ambapo wazee wetu walipigania Tanganyika ili iwe mwisho wa harakati zao.

Wazee wetu wote na historia ni shahidi walitambua kuwa Uhuru wa Tanganyika ulikuwa ni mwanzo tu wa kufikia lengo kamili nalo ni kutokomeza ukoloni, kurejesha utu wa watu wetu na kuwarudishia Waafrika umoja wao ili kuweza kujenga taifa jipya, kubwa na la kisasa ambamo watoto wake wanaishi kwa furaha na wakifurahia matunda ya uhuru.

Ni kwa sababu hiyo, ninawatakia Watanzania wote kheri na fanaka za Uhuru wetu na kwa pamoja tuzidi kupigania Tanzania ambayo ni nchi tuliyojiundia sisi wenyewe ambayo ilitokana na misingi ya harakati za uhuru. Anayepigania kuivunja Tanzania hapiganii Utanzania wetu kwani hana msingi wa historia unaoweza kumuunga mkono. Anayeogopa shirikisho la Afrika ya Mashariki hana msingi wa historia – Watanzania hatujawahi kuogopa Shirikisho la Afrika ya Mashariki!; Aneyataka kuvunja Muungano anataka kitu ambacho hakimo katika historia hiyo.

Naifurahia Tanzania, siyo Tanganyika. Kama watu wanataka jina tu la Tanganyika au mabadiliko wanaweza kufanya hivyo bila kutaka kuvunja na kulikana wazo la Tanzania.

Makala ya Lula wa Ndali Mwananzela, Raia Mwema

Advertisements

About zanzibarpost

Independet Online media in and for Zanzibar
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.