Fat-hu Zinjibari

Zanzibar

Kufuatia sui-tafahumi ya miaka nenda miaka rudi katika dola ya Zanzibar, ambayo ilipelekea kudamirika na kupoteza hadhi yake ya asili, Wazanzibari walipigana vita visivyokuwa vya kumwaga damu na hatimae kuikomboa dola ya Zanzibar, katika tukio hili nnaloliita Fat-hu Zinjibari. Vita hivi vilivyopiganwa na makabila mawili yaliyochipukia hivi miaka ya karibuni tu, -lile la Wahafidhina na la Wanamageuzi- vilipiganwa mwanzoni kwa sirisiri na kisha dhahiri. Leo hii, kwa uwezo wa Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo, vita hivi vimemaliza kwa kuwapa ushindi Wanamageuzi, ambao tabaan, ndilo kabila kubwa kwa sasa nchini hapa.

Nipo katika mji mkuu wa Zanzibar. Ni siku ya Ijumaa ya tarehe adhimu katika historia ya Zanzibar. Kiujumla hali ya hewa ni tofauti na siku zote zinazokumbukwa na wakaazi wa nchi hii. Sura za watu zinaonekana kumetameta kwa furaha. Wadogo kwa wakubwa wanaonekana na furaha, wakiwa wamevalia mavazi rasmi kwa ajili ya siku hii, na kwa mujibu wa mkaazi mmoja wa hapa, mavazi haya yalidariziwa siku nyingi zilizopita, tangu zilipoonekana dalili za ushindi, ingawa dalili zenyewe nazo hazikuwa mutawaliya. Zilikuwa ni za kupwa na kujaa, ambazo ziliwakatisha tamaa wengi na kuwatia jakamoyo la roho.

Majiani watu wamesambaa wakisalimiana na kupongezana kwa ushindi huu ambao haukuitwa ushindi wa Wanamageuzi, bali ushindi wa Wazanzibari kwa Wazanzibari. Sijui walikusudia nini. Anga la mji ni kama lililopuliziwa uturi wa Imperial Majesty, uturi ghali kati ya nyuturi zote duniani. Katika nguzo za taa za umeme kunanin’ginia mashada ya mauwa yaliyofumwa kwa ustadi, yenye mchanganyiko wa asumini, mawaridi, viluwa na mauwa mengine ambayo harufu yake ikichanganyika na ile ya Imperial Majesty inawafanya wakaazi wa mji huu wawe na kitu chengine cha kusifia nchi yao mpya. Harufu isiyopatikana pengine popote duniani.

Kwa mbali naona kikundi cha wanamadrasa wa Almadrasatu Hurriyyah wakiwa na twari zao njiani. Wamevalia kanzu na vilemba vya haggal. Hawa wanaimba kasida ya kiarabu, yenye mahadhi na naghma zinazofanana na ile nyimbo iliyokuwa ikiimbwa hivi karibuni nchini hapa “…tunataka nchi yetu sasa tumechoka…” wamejipanga kwa safu kama wanaopigana vita vya mikuki.

Kuna mengi bado ya kuyaona na kuyasimulia siku hii ya leo, ambayo kwa sasa mtaniwiya radhi sitawasimulia zaidi. Nakimbilia viwanja vya Maisara, kuskiliza hutuba ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Lakini sitawatendea haki kama sitawaambia yaliyopo Jaws Corner, Lebanon Brothers na barza nyingine za mjini hapa. Baraza zote za barza hizi kumejaa sahani za halua na mideli ya kahawa (mideli, si mabirika) ambavyo ni mahsusi kwa kila mpita-njia na mkaazi wa hapa. Viwanja vya Kisonge nako kumewekwa TV kubwa, flat screen, inayoonesha matukio yanayojiri hapa na pale kote visiwani Zanzibar. Hapa napo pia pamefunikwa na furaha za kweli. Hapako kama palivyozoweleka. Katika pitapita zangu zote hizo, sijabahatika kuona bendera ya chama chochote cha siasa ikipepea, zaidi ya bendera mpya ya Zanzibar.

Nipo Maisara sasa. Nimechelewa kidogo, hivyo nimekuta uwanja umeshafurika. Barabara ielekeayo Mnazi mmoja imejaa magari yaliyoegeshwa yakitokea Makunduchi, Donge, Fumba na sehemu nyingine zote za kisiwa cha Unguja. Baadhi ya magari haya, naambiwa, yemefika hapa tangu jana usiku ili kuwahi fursa hii adhimu ya tukio hili la kihistoria. Vikosi vya JWZ ndio vinamalizia kuimba wimbo wa Taifa la Zanzibar. Raisi wa JWZ ameshamaliza kuwasalimia watu, kama ilivyo ada ya protokoli na sasa ndio anaanza hutuba yake. Tumsikilize:

Ndugu wananchi,
Ile siku muliyokuwa mukiisubiria kwa hamu leo ndio imefika. Terehe ya leo itaendelea kubaki katika vitabu vya historia kuwa ni siku iliyotangazwa upya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, iliyopatikana kufuatia hatua ya kupitiwa upya na kukarabatiwa kwa maridhiano ya viongozi na wananchi wa iliyokuwa Jamhuri ya Muungano.

Wengi wetu tutakumbuka kwamba taifa letu limepita katika vipindi vigumu sana, hasa katika miaka hamsini iliyopita ambapo matukio mengi makubwa ya kisiasa yalimaanisha kudamirika kwa taifa letu la Zanzibar. Lakini juu ya yote muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Muungano haukuwa na sura na misingi imara ya kuweza kutufikisha tulipopadhamiria, ndio hatma yake leo tumefikia hatua hii ya kuitangaza dola na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, lakini bado tukiwa na mahusiano na ushirikiano mzuri na ndugu zetu na majirani zetu.

Ndugu wananchi,
Ni jambo la kushukuru kwamba tofauti na nchi nyingine za barani Afrika, kama Eritrea na Sudani ya Kusini, Zanzibar imeweza kuirejesha hadhi yake bila ya kutumia mtutu wa bunduki wala umwagaji damu. Hichi ni kiwango kikubwa cha demokrasia iliyotukuka na uelewa wa viongozi wetu wa iliyokuwa Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja, lakini pia kwa ufahamu wenu nyinyi wananchi wetu, mukaweza kustahmili misukosuko yote iliyowapata wakati wa kuratibu na kuelekea kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Kwa hilo sina budi kuwapongeza!

Nikiwa kama mlezi wa Taifa hili,, nina furaha isiyo kifani kuweza kuwa mshiriki kikamilifu katika kukiendea mbio na kuwapatia wananchi wangu kile walichokililia kwa muda mrefu. Lakini sina budi kukiri kwamba katika hili mimi nilikuwa dereva tu, ila watengezaji wa gari na waandaaji wa njia ni nyinyi wananchi wangu na viongozi wetu shupavu waliosimama kidete kuwaunganisha wananchi na kujua lengo na dhamiri yao kwa maslahi ya taifa lao. Nyinyi na wao nawashukuruni sana.

Ndugu wananchi,
Bila shaka mutakuwa mumebaini kwamba safari tuliyokuwanayo ilikuwa ni safari ndefu sana, yenye kuchosha na kukatisha tamaa. Safari yetu hii bado haijafika mwisho wake, bali yote hayo yalikuwa ni maandalizi ya safari yenyewe. Kwa maneno mengine, kipindi chote hicho cha kuipigania Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilikuwa ni kama kulea mimba. Na waswahili tunasema kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana. Mwana ameshazaliwa, kinachofuatia ni malezi ya mwana huyo, ambayo hayatakuwa na mwisho.
Katika hili la malezi, naomba niweke bayana kwamba halitakuwa jukumu langu mimi tu kama mlezi wa taifa hili, lakini kila mmoja wetu kwa nafasi yake atakuwa na wajibu na dhamana ya kuijenga, kuilinda na kuipenda Zanzibar. Hili lijengeke katika misingi ya kwamba sisi sote ni wachunga, na kila mmoja wetu ataulizwa, kwa nafasi yake, juu ya kile alichokichunga.

Wapendwa wananchi,
Katika kipindi cha takriban nusu karne iliyopita, Zanzibar ilidorora si tu katika medani za kisiasa, lakini pia, na hasa, katika suala zima la uchumi. Sababu kubwa tulizozinyooshea vidole ni kutokuwa kwetu na uwezo wa kuingia katika mikataba na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa, lakini tulilolisahau, na ambalo lilikuwa na athari kubwa ni uwajibikaji mbovu na suala zima la rushwa. Kwa kiasi kikubwa rushwa iliturudisha nyuma kimaendeleo tukajikuta jitihada zetu za kuimarisha uchumi zinakwama njiani.

Katika kuijenga Zanzibar mpya rushwa haitakuwa na nafasi hata ndogo. Vyanzo vyote vya mapato ya serikali vitakuwa chini ya usimamizi mzuri na wa uadilifu. Hilo linawezekana, kwa kuwa serikali yenu imedhamiria kuweka viwango vizuri vya mishahara vitakavyomtosheleza mwananchi kuishi bila ya wasiwasi, na bila ya kutegemea rushwa. Vyombo vya kusimamia sheria, polisi na mahakama, navyo vitaboreshwa ili mwenye haki apate haki yake, na mhalifu kupata adhabu inayostahiki.

Ndugu wananchi,
Suala la mazingira ni miongoni mwa mikakati tuliyojiwekea katika kuijenga Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hatuna budi kujitofautisha sisi na wengine katika suala la usafi, lakini pia kutofautisha baina ya tulikotoka, tulipo na tuendako. Kwa kuwa tumedhamiria kujenga taifa jipya, ni lazima taifa letu hili liwe safi katika hali zote. Na usafi, kama ulivyo uchafu, huanza katika sehemu ndogo sana, na athari yake kutapakaa katika jamii yote. Hivyo hatuna budi kulipa kipaumbele suala la usafi kwa kuanzia na sisi wenyewe miilini myetu, vyumbani mwetu, majumbani mwetu na kisha mitaani mwetu.

Kila mmoja wetu, bila kusimamiwa wala kuhimizwa, awe ni mlinzi mzuri wa mazingira yetu. Wazee wawe ni mifano bora kwa watoto katika udhibiti wa takataka za majumbani, kama watakiwavyokuwa walimu kwa wanafunzi wao. Somo maalum lianzishwe maskulini kuwafunza watoto wapi na vipi watupe taka. Binafsi nitajitolea mimi pamoja na mawaziri wangu kwa utaratibu maalumu siku moja katika kila mwezi kwa ajili ya kusaidia kuweka hali ya usafi katika mazingira ya miji yetu na vijijini.

Ndugu wananchi,
Kama ilivyo kwa mambo mengine, suala zima la maendeleo ya nchi linahitaji mashirikiano na moyo wa dhati wa kujitolea. Kila mmoja wetu, kuanzia mtoto mpaka mzee ana uwezo wa kuchangia kwa njia moja au nyingine katika kuleta maendeleo, iwe ya kiuchumi au ya kijamii. Tuzitumie fursa zote tulizonazo ili kuhakikisha katika kipindi hiki cha mwaka wa kwanza Zanzibar inakuwa ni nchi ya kupigiwa mfano katika ukuaji wa uchumi, si tu kwa Afrika Mashariki, lakini Afrika yote kwa jumla.

Mwakilishi wetu wa kudumu katika Umoja wa Mataifa tayari yupo mjini New York kwa kuanza kazi rasmi ya kuitangaza Zanzibar na kufanya mazungumzo ya uhusiano na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa. Wajumbe wengine tumeshawatuma katika nchi mbalimbali ili kutafiti maendeleo katika nyanja husika tayari kuyafanyia kazi.

Kwa kumalizia, naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi zote ambazo zimeonesha nia ya kujenga urafiki na mahusiano mema na Zanzibar. Tunazipongeza jumuiya na taasisi zote ambazo zimetoa mialiko ya kuiomba Zanzibar kuwa mwanachama, na sisi tunaahidi tutayatahmini maombi hayo na kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kuyatimiza malengo yetu, na aijaaliye Zanzibar iendelee kuwa nchi ya amani na utulivu daima.

Mungu ibariki Zanzibar,
Mungu wabariki Wazanzibari
Ahsanteni

Raisi amemaliza hutuba yake, anashuka jukwani na kusalimiana na viongozi na wananchi waliokuwa wakimskiliza kwa makini.

Wakati nilipokuwa nikiyasimulia haya, nilizisikia sauti za bezo na kebeho zikiniambia ati naota. Nazambia hapana, sioti. Hii ni kweli isiyo na shaka. Ni kweli isiyosutika. Na hata kama ni kweli naota (nasisitiza kwamba sioti), kwani ni dhambi kuota. Na hata kama ni dhambi, sitakwenda kuwa wa kwanza na pekeyangu kuhukumiwa. Bila ya shaka nitakwendashikana mkono na yule mwanakindakindaki wa Zanzibar, Mohammed Ghassany, aliyewahi kuota ndoto hii:

Naota ni mkoloni, naitawala Ulaya
Britini, Jarumani, Uswidi na Rumania
Zote zimo mikononi, ninazo nazikalia

Naota nipo kitini, na jeshi kubwa la riya
Wazungu ni masikini, mararu ‘mejivalia
Dhaifu wa hali duni, mithali wana wakiwa

Dola kubwa Marekani, naota lishapotea
Teksasi, Kalifoni, Florida zimevia
Nami nina usukani, UNO yanisujudia

Kusini, kaskazini, Afrika, Arabia
Bendera mlingotini, ya Zenji inapepea
Watwani Nurul-eni, imekuwa Empaya

Nayaota makoloni, Amerika na Ulaya
Wamechoshwa na uduni, uhuru wapigania
Waingia misituni, kusudi kuniondowa

Japo sitaki moyoni, napaswa kuwaachia
Walakini masikini, watashindwa jiinua
Nawabambikiza deni, wazidi nitegemea

Ninashituka njozini, akili yanirudia
Kumbe nipo kitandani, kunguni wanibugia
Zenji yaja fikirani, isi hata

Zanzibar

uraia!

Na Hamad Hamad, Copenhagen

Advertisements

About zanzibarpost

Independet Online media in and for Zanzibar
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.