Jinsi Moyo alivyowasuta wanaojaribu kuuvunja Umoja wa Wazanzibari

Mzee Hassan Nassor Moyo, mmoja wa waasisi wa CCM na mpigania muungano wa mkataba baina ya Tanganyika na Zanzibar

WIKI iliyopita nilizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi kama Zanzibar ya leo kuwa na siasa za umoja badala ya kuwa na siasa za mivutano. Hii ni mivutano yenye kutishia amani ya nchi na hupaliliwa na vyama vya kisiasa.

Niligusia pia juu ya umuhimu wa kuiweka nchi mbele badala ya kuweka sera za chama — kuyapa kipaumbele maslahi ya kitaifa badala ya maslahi ya kichama. Kwa ufupi, nikizungumzia juu ya haja ya kuwa na vuguvugu la umoja wa kizalendo.

Kwa sadfa Jumamosi iliyopita palifanywa kongamano kubwa mjini Unguja, kongamano ambalo ni mfano mzuri wa siasa za umoja, nilizokuwa nikizizungumzia. Kongamano hilo, lililokuwa chini ya uwenyekiti wa Profesa Abdul Sheriff (mmoja wa wanahistoria waliobobea barani Afrika) liliandaliwa na Kamati ya Maridhiano chini ya uwenyekiti wa Hassan Nassor Moyo.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo kwa upande wa CCM, ni Waziri asiye kuwa na Wizara Maalum na Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himidi na Eddy Riyami ambaye ni mkereketwa wa CCM. Kwa upande wa CUF walikuwamo Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Abubakar Khamis Bakary, Mkurugenzi wa Uenezi wa CUF, Salim Bimani na Ismail Jussa Ladhu, Mwakilishi wa CUF wa Mji Mkongwe ambaye wiki iliyopita alijiuzulu wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu wa CUF.

Hawa Wazanzibari sita wamekuwa kama gundi inayoishikilia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar na kuhakikisha kwamba mshikamano na umoja wa Wazanzibari unaendelea kwa manufaa ya taifa letu. Kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Bwawani, lilikuwa ni la kihistoria. Hapajawahi katika historia nzima ya kisiasa ya Zanzibar kufanywa mjadala wa kitaifa kama uliofanywa kwenye mkusanyiko huo na kuhudhuriwa na watu kutoka vyama tofauti vya kisiasa na kutoka taasisi na jumuiya mbalimbali za Zanzibar zikiwa pamoja na za kidini.

Ijapokuwa kongamano hilo lilikuwa la kwanza la aina yake kuandaliwa visiwani, inasikitisha kwamba vyombo vingi vya habari vya Tanzania Bara vililibeza. Lile tangazo la pamoja la kongomano hilo halikusambazwa na vyombo hivyo vya habari kama inavyostahili. Zanzibar kwenyewe kongomano hilo halikuweza kupuuzika. Yaliyokuwa yakizungumza na kujadiliwa kwenye kongamano hilo, yalirushwa na stesheni za televisheni zisizo za Serikali, na yalitangazwa na steshini za redio zilizo huru na hata kwenye majukwaa mbadala na mitandao ya mawasiliano ya kijamii.

Mada ya kongamano ilikuwa ‘Nafasi ya Zanzibar Katika Mchakato wa Katiba Mpya.’ Jambo lililotia moyo katika mjadala huo ni kwamba hakukuwa na maoni yaliyokuwa yakikinzana wala hakuzuka yeyote aliyetoka kwenye mstari wa maudhui. Hilo pekee lilizidi kuthibitisha jinsi Wazanzibari hii leo wanavyozidi kuwa na umoja wa fikra kuhusu mstakabali wao.

Jengine lililotia moyo ni kuwaona waliokuwa wakichangia kwenye mdahalo huo kuwa ni watu wa itikadi tofauti za kisiasa na kutoka vyama na jumuiya mbalimbali lakini wote wakishikilia uzi mmoja: uzalendo wa Wazanzibari.

Ilifurahisha kumsikia Moyo akiwajibu baadhi ya wazee na viongozi wenzake wa CCM-Zanzibar waliokuwa wakijaribu kumkwaruza na kumvunjia heshima yake kwa sababu ya msimamo wake kuhusu mustakabali wa Zanzibar. Moyo, mwenye kadi namba 7 ya CCM, alizungumzia zaidi juu ya Maridhiano yaliyosaidia kuuleta huu umoja uliopo sasa Visiwani.

Tukimwacha Moyo, mzee mwingine aliyezungumza alikuwa Salim Rashid aliyekuwa katibu wa mwanzo wa Baraza la Mapinduzi, na aliyewahi kuwa waziri na balozi wa Tanzania nchini Guinea na Ethiopia. Alitoa mbiu mpya ya kuwataka Wazanzibari wawe na ‘Umoja wa Pamoja’ kupigania maslahi yao.

Vigogo wengine waliozungumza katika kongamano hilo, walikuwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee, Amiri Mkuu wa Jumiki, Sheikh Msellem Ali Msellem, Mansour Yusuf Himidi, Mwenyekiti wa ZAHILFE Kassim Hamad Nassor, Mwakilishi wa WAHAMAZA, Salma Said, Mwakilishi wa UKUWEM Dk Mohamed Hafidh, Rais wa Zanzibar Law Society, Salim Toufiq na Khalid Gwiji ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana wa Umoja wa Kitaifa.

Mwingine aliyeusisimua mkutano huo kwa mchango wake, alikuwa Padri Emmanuel Masoud wa Kanisa la Kianglikana kutoka Pemba, ambaye alisisitiza kwamba aliyokuwa akiyasema yalikuwa maoni yake na hayayawakilishi yale ya Kanisa lake. Kasisi Masoud alisema kwamba yeye ni Mzanzibari kutoka Pemba mwenye kuyaunga mkono Maridhiano ya Rais Mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF. Aliongeza kwamba yeye vilevile anaunga mkono Muungano wa Mkataba na anataka Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili.

Hamna shaka yoyote kwamba Maridhiano ndiyo yaliyowezesha pakapatikana hali ya amani na utulivu Zanzibar. Na inavunja moyo tunapowasikia baadhi ya viongozi wa CCM na baadhi wakereketwa wakongwe wa chama hicho wakitia fitna ambazo hatima yake itakuwa ni kuirejesha Zanzibar kule ilikotoka kwenye chuki za kisiasa na kikabila, uhasama na umwagaji wa damu.

Bila ya shaka ni kweli kwamba panapokuwako siasa za umoja, haimaanishi kwamba tofauti za vyama zinayayuka na kutoweka moja kwa moja papo kwa papo. La. Tofauti hizo huendelea kuwako, lakini zinakuwa zinawekwa kando na hazitiliwi sana maanani. Kinachotiwa maanani ni maslahi ya nchi. Katika mfumo kama huo, nchi huja mwanzo halafu ndio vinakuja vyama au vivyama.

Inapokuwa lazima tofauti hizo zijitokeze, basi hujitokeza kwa njia za kistaarabu na mazingira ya kuvumiliana.

Lakini hivyo sivyo wanavyofanya baadhi ya wapinzani wa Maridhiano. Daima kunakuwa na hatari kwamba siasa za umoja zinapochezwa, huenda pakazuka vidudumtu au vitambakwiri vitakavyotaka kuuvunja huo umoja uliopo. Potelea mbali nchi iteketee au iangamie, madhali wao wanapata maslahi yao. Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, tunaiona hatari hiyo ikitoka kwa wahafidhina wa CCM-Zanzibar.

Wote hao wanakuwa wanafanya dhambi kwa sababu wanakuwa wanakwenda kinyume na mkondo wa kihistoria. Kwa wakati huu tulio nao sasa, historia ya Zanzibar inashurutisha kwamba lazima pawepo na siasa za umoja. La sivyo basi, visiwa vya Zanzibar vitaangamia.

Katika hali iliyoko Zanzibar, siasa za umoja si jambo linalohitajika tu, bali siasa hizo zinakuwa ni kama silaha ya kutumiwa kupigania haki katika vuguvugu la kidemokrasia. Aidha, siasa za aina hiyo zinakuwa zinazitoa kasumba za kiitikadi zinazoshadidiwa na uchama. Kasumba hizo hutumiwa na viongozi wakorofi kuwalewesha wafuasi wa vyama vyao.

Kwa kweli siasa za umoja zinakuwa na uwezo wa kuwafungua huru wananchi na kuwafanya wasifungwe tena na pingu za kichama. Lengo lao linakuwa kupigania tu nchi yao na maslahi ya nchi yao na ya vizazi vyao. Faida nyingine ya siasa za umoja, ni kwamba zinaweza kuwafungua macho na kuwazindua wananchi waliozugwa kwa itikadi za kichama. Wanaowazuga hao wananchi aghalabu huwa ni wanasiasa wanaofanya hivyo kwa makusudi ili wafuasi wao wasiweze kujiamini na kuwa na msimamo wa kuiweka nchi mbele.

Wanasiasa hao wanapowaona wafuasi wao wamesimama kidete na hawateteleki, basi huanza kupapatika. Na wakianza kupapatika, ndipo wanapotumia vitisho kuwatisha wafuasi wao. Tumeyashuhudia hayo yakitokea Zanzibar pale baadhi ya viongozi wa CCM wenye msimamo ulio kinyume na ule wa wafuasi wao, wanapoanza kuwatishia baadhi ya wenzao wenye msimamo tofauti na wao kwamba watawafukuza chamani. Hawaishii hapo, bali wanauvua ustaarabu wao na wanaanza kuwatupia wenzao kila aina ya matusi.

Hiyo ni ishara ya kwamba viongozi hao wanaojiona kuwa ni wababe, kwa kweli wamekuwa muflisi wa kisiasa. Si hayo tu, bali wanajiona kuwa wanazama baharini na hawajui washike nini ili wajiokoe; ndipo wanapovamia vitisho na kuanza kuvitumia dhidi ya wenzao. Na wanapotumia hivyo vitisho ndipo wanapozidi kujikashfu na kuonekana kuwa si chochote bali ni ‘chui wa karatasi’ chambilecho Mwenyekiti Mao.

Kongamano la Jumamosi iliyopita, limethibitisha kwamba siasa za umoja zinaweza zikatumiwa kwa mafanikio kuwaunganisha wananchi na kuwafanya wajipange kupigania maslahi yao. Kadhalika siasa za aina hiyo, zinapokuwa zinaanza kuiva na kupevuka kama zilivyo sasa Zanzibar, huwavutia wananchi wengi zaidi. Hata wale wasiokuwa zamani wakijihusisha na siasa, huanza kujiingiza uwanjani kupigania maslahi ya taifa lao.

Hiyo ndiyo sababu ya kwa nini ukumbi uliofanyiwa kongamano ulifurika umati, wengi wao wakiwa vijana. Kwamba wengi waliohudhuri kongamano hilo walikuwa vijana ni jambo jingine lenye kutia sana moyo kwa vile mustakabali wa nchi yao, umo mikononi mwao.

Juu ya hayo yote, hali tuliyonayo Zanzibar ni tata. Ina mazongezonge mengi na si sahali au nyepesi hata kidogo. Hivyo, vijana lazima watambue kwamba mapambano yoyote ya kuleta mageuzi huwa na hatua nyingi za kupitia. Kwanza huanzia na fikra za kutaka kuleta mageuzi katika jamii fikra ambazo hutokana na shauku ya umma ya kutaka kuwa huru. Fikra kama hizo, daima huwachemsha wananchi wenye kuipenda nchi yao. Kwa taratibu watu huanza kushawishika na kujitolea kuchukua hatua nyingine za kusonga mbele na mapambano.

Kwa sasa Zanzibar imekwishaipita hatua hiyo. Muhimu ni kwamba vijana wasipoteze dira wala wasijiachie wakayumbishwa na wanasiasa wanaotaka kuyarejesha ya kale na kuitokomeza nchi.

Makala ya Ahmed Rajab, RaiaMwema Toleo la 262

 

Advertisements

About zanzibarpost

Independet Online media in and for Zanzibar
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.